Header Ads

Mkenya Mary Keitany anapanga kuwatumia wanaume mbioni London Marathon

Mary Keitany

Mkenya Mary Keitany amesema atawatumia wanariadha wanaume kumsaidia kuongeza na kuendeleza kasi katika jaribio la kuvunja rekodi ya Paula Radcliffe.
Keitany anataka kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za marathon za "jinsia mchanganyiko" katika mbio za London Marathon Aprili.
Rekodi hiyo ya saa mbili, dakika 15 na sekunde 25 imedumu kwa miaka 15 bila kuvunjwa.
Shirikisho la riadha duniani hutambua rekodi mbili za dunia - jinsia mseto na wanawake pekee.
Mwaka jana, Keitany alivunja rekodi ya wanawake pekee ambayo pia ilikuwa inashikiliwa na Radcliffe baada ya kuweka muda bora zaidi duniani wa 2:17:01.
Keitany, 36, anatumai kwamba kila kitu kitakuwa sawa wakati huo akijaribu kuvunja rekodi hiyo.
"Nafahamu kwamba rekodi hiyo iliwekwa na Paula Radcliffe uwanja huu 2003 na yeye ni maarufu sana Uingereza," aliongeza bingwa huyo mara tatu wa London Marathon.
"Lakini ninataka kuwavutia wakazi wa London wanishangilie katika jaribio hili langu na kunisaidia kutimiza lengo hili.
"Kwa kuwa na wanaume wa kunisaidia kuongeza na kudumisha kasi, nitakuwa na usaidizi kote mbioni."
Mbio hizo zitaandaliwa Jumapili 22 Aprili.
Mwaka 2017, Keitany alifika nusu ya mbio hizo akiwa dakika moja mbele ya muda wa Radcliffe wa 2003 lakini kasi yake ikapungua baada ya hapo.
Amesema amekuwa akipanga kuvunja rekodi hiyo kwa miaka mingi.

No comments